
Mwenyekiti wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB), Mhandisi Joseph Nyamhanga, amezitaka Taasisi za Umma kuzingatia sheria ya ununuzi wa umma ya mwaka 2023 na kanuni zake za mwaka 2024, ambazo zinaelekeza kuwa mikataba ya miradi ambayo haizidi shilingi BilionI 50 inatakiwa itekelezwe na Makandarasi wazawa.
Amesema hayo wakati wa mwendelezo wa ziara ya Bodi ya Wakurungenzi na Menejimenti ya CRB inayofanywa katika mikoa minne ya Kanda ya kaskazini ambayo ni Manyara, Arusha, Kilimanjaro na Tanga kwa lengo la kukagua utendaji kazi wa Makandarasi na utekelezaji wa Miradi.
Mhandisi Joseph Nyamhanga, ametumia fursa hiyo kuzitaka kampuni za kigeni zinazojenga miradi nchini, kutoa kandarasi ndogo (sub-contractors) zenye thamani kubwa ya fedha kwa Makandarasi wazawa ili miradi hiyo iwajengee uwezo.
Akitoa taarifa kwa wajumbe wa Bodi hiyo pamoja na Menejimenti ya CRB, Meneja wa mradi Mhandisi Sakina Mohammed amesema kuwa mradi huo wa usambazaji wa umeme vijijini (REA) ni wa miaka miwili na utasambazwa katika vitongozi 135 vya mkoa wa Kilimanjaro na mpaka sasa umefikia asilimia 11.6 ya utekelezaji wake.
Katika hatua nyingine Bodi ya Wakurugenzi pamoja na Menejimenti ya CRB, walitembelea mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta ghafi wenye thamani ya shilingi trilioni 1.4 unaotekelezwa na Mkandarasi China Petroleum Pipeline Engineering Co. Ltd (CPP) katika kijiji cha Misino, Wilaya ya Handeni Mkoani Tanga na kuridhishwa namna mradi huu unavyotekelezwa.
Akizungumza mara baada ya ukaguzi wa mradi huo Mwenyekiti wa Bodi ya CRB Joseph Nyamhanga amempongeza Mkandarasi huyo kwa kuajiri watanzania kwa zaidi ya asilimia 70 pamoja na kutoa fursa ya kandarasi ndogo (Sub – Contractors) kwa Makandarasi wazawa, ambapo pia amewataka Makandarsi hao kukamilisha mradi kwa viwango na kwa wakati.
Akitoa taarifa ya mradi huo Willhel kiria ambaye ni meneja wa mazingira katika mradi huo,amesema mradi huo pia unazingatia uhifadhi wa mazingira kwani utekelezaji wake hauharibu miundombinu iliyopo.
Wajumbe hao wa Bodi pamoja na Menejimenti ya CRB, pia wametembelea kambi namba 16 ya Mkandarasi China Petroleum Pipeline Engineering (CPP) iliyopo katika Wilaya ya Muheza mkoani Tanga ambapo wameshuhudia maandalizi ya awali ya kambi ikiwa na utayari wa kuanza ulazaji wa bomba hilo la mafuta ghafi utakao anzia Kabaale - Hoima nchini Uganda na kuishia Chongoleani mkoani Tanga nchini Tanzania.
Wajumbe wa Bodi pamoja na Menejimenti ya CRB wanaendelea na ziara ya kukagua miradi mbalimbali katika mikoa ya kanda ya kaskazini,ambapo wanatarajia kukamilisha Ziara yao jijini Tanga.