![](https://www.itv.co.tz/sites/default/files/styles/large/public/field/image/EFD.jpg?itok=77jL8wDH)
Hatimaye wataalamu wa masuala ya Teknolojia ya upashanaji habari na wa taasisi zingine za serikali wamemaliza sakata la mashine zakutolea risiti za kielektoniki zilizokuwa zimepata hitilafu na kushindwa kutoa risiti kwa takribani wiki tatu sehemu mbalimbali nchini ambapo kwa sasa zimepona na zimeanza kufanya kazi.
Akizungumza wakati akifanya ziara ya kutembelea maduka mbalimbali jijini Dodoma kwa lengo la kukagua kama wafanyabishara wanatoa risiti Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Ashatu Kijaji amesema mashine zilizokuwa zikisumbua sasa zimerekebishwa na kuwataka kutumia mashine hizo kwa lengo la kukusanya mapato.
Kwa upande wake Kamishna wa kodi za ndani kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA Bwana Eleja Mwandumbya amesema awali mashine hizo zilipata hitilafu ya kiufundu ambapo amesema hitilafu hiyo ilitokana na kufeli kwa mojawapo ya kifaa cha kuchakata taarifa.
Baadhi ya wafanyabiashara wamekiri kuwa hapo awali mashine hizo zilikuwa zikifeli kutoa risiti ambapo kwa sasa zimeanza kufanya kazi ambapo wameiomba serikali kudhibiti tatizo hilo lisijirudie tena.