Wadau mbalimbali wametaka juhudi za makusudi ziwepo ili kuhakikisha mnyama adhimu aina ya sokwe mtu ambaye yupo katika hatari ya kutoweka kutokana na shughuli za kibinadamu anaendelea kuwepo kwa manufaa ya kizazi cha sasa na baadae.
Wamesema wakati wa Maadhimisho ya siku ya sokwe mtu duniani kuwa mnyama huyo ambaye kwa sasa anapatikana katika hifadhi za taifa za milima ya Gombe na Mahale mkoani Kigoma pamoja na hifadhi ya taifa Rubondo na katika misitu iliyohifadhiwa , kuwa shughuli za kibinadamu ambazo zinaendelea zinatakiwa kuratibiwa vizuri ili kutoendelea kuathiri makazi ya sokwe mtu ambao kwa sasa wamekuwa sehemu ya utalii na kuliingizia taifa fedha.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa sayansi ya uhifadhi kutoka taasisi ya Jane Goodal Dr.Shadrack Kamenya amesema ikiwa mazingira yataendelea kuharibiwa sokwe mtu watapotea na kwamba serikali za vijiji zina wajibu wa kuhifadhi misitu na kuwachukulia hatua watu wanaofanya shughuli za kibinadamu zinazoathiri mazingira kwa sababu sokwe hutegemea chakula kutokana na uhifadhi bora wa mazingira.