Wachimbaji watano wa madini ya dhahabu mkoani Geita wamefukiwa na kifusi huku mmoja akifariki dunia na watatu wakiokolewa na kukimbizwa hospitali ya mkoa na mmoja hajulikani alipo baada ya mgodi walipokuwa wakichimba dhahabu kuporomoka na kuwaangukia.
ITV ilifika eneo la Magema ambapo ajali hiyo imetokea na
kushuhudia mamia ya wachimbaji wadogo kwa kushirikiana jeshi la zima moto na uokoaji wakiendelea na zoezi la uokoaji.
Mtaalamu wa uokoaji kutoka jeshi la zimamoto na uokoaji mkoa wa Geita Inspekta Stanley Luagu anasema tayari wamefanikiwa kuwaoka wachimbaji wanne huku wakiendelea na zoezi la kumtafuta mmoja anayesadikiwa kusalia chini ya mgodi.
Kamanda wa polisi mkoa wa Geita Mponjoli Lotson amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kusema mamia ya wachimbaji hao wamevamia na kuchimba kinyemela sehemu ya mgodi mkubwa wa GGM huku akiwataka wachimbaji hao kuchukua tahadhari.