Back to top

Rais Mwinyi atoa neno kuhusu muungano.

26 April 2022
Share

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema kuwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar uliozaa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ukiwa unatimiza miaka 58 bado unaendelea kuimarika kwa kiasi kikubwa.


Rais Dk. Mwinyi aliyasma hayo wakati akitoa salamu zake za kusherehekea miaka 58 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kupitia vyombo vya habari Ikulu Jijini Zanzibar.


Katika salamu zake hizo Rais Dk. Mwinyi alieleza kuwa ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania bado wananchi wake wako pamoja hatua ambayo imeweza kuleta mafanikio makubwa ndani ya miaka 58 ya Muungano huo.


Alisema kwamba Tanzania bila ya Muungano sio kitu ambacho kinaweza kufikiriwa kwani Watanzania walio wengi wamezaliwa ndani ya kipindi cha Muungano hivyo, alitoa wito kwa wananchi wote kuendelea kuuezi na kuudumisha kwa faida ya kizazi kiliopo na kijacho.


Aliongeza kuwa Muungano uliopo hivi sasa ni wa damu zaidi kuliko Muungano wa vitu kwani wananchi walio wengi wana uhusiano wa Zanzibar na Tanzania Bara hivyo, wote ni wamoja.


Rais Dk. Mwinyi alisema kwamba licha ya wananchi wake kuchanganya damu pia, kuna mafanikio makubwa yaliopatikana kupitia Muungano hususan biashara kwani bidhaa nyingi zinazotumika Zanzibar zinatoka Tanzania Bara.


Alisema kuwa mbali ya muunganiko wa watu na biashara pia, kumekuwa na mafanikio makubwa katika suala zima la ulinzi na usalama ambapo katika kipindi chote cha miaka 58 ya Muungano kumekuwa na amani na usalama.