
Serikali imezitaka Taasisi zote za umma na binafsi nchini zinazoandaa chakula na kulisha watu zaidi ya 100 kwa siku, kusitisha matumizi ya kuni na mkaa ifikapo Januari 31, 2024, huku zile zinazoandaa kwa ajili ya watu zaidi ya 300 kwa siku, zikitakiwa kusitisha ifikapo Januari 31, 2025.
.
Akizungumza na waandishi wa habari leo April 12, 2023, Jijini Dodoma, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dkt.Selemani Jafo, amezihimiza taasisi hizo kutumia nishati mbadala ambayo ni safi kwa ajili ya kupikia.
“Kwa mamlaka niliyopewa chini ya kifungu cha 13 cha sheria ya usimamizi wa mazingira, sura ya 191, natoa katazo Kwa Taasisi zote za umma na binafsi Tanzania Bara zinazoandaa chakula na kulisha watu kuacha matumizi ya mkaa na kuni,” amesisitiza Dkt. Jafo.