Back to top

WANANCHI FANYENI UCHUNGUZI WA AWALI KWA KUPIMA SARATANI YA MATITI.

01 October 2023
Share

Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amewataka wananchi  kufanya uchunguzi wa awali wa kupima Saratani ya Matiti ili kujua hali zao na kupata matibabu mapema kwa wenye changamoto hiyo

Waziri Ummy ameyasema hayo leo Octoba Mosi, 2023 wakati akimuwakilisha Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango kwenye Maadhimisho ya Mwezi wa Saratani ya Matiti yaliyofanyika katika viwanja vya Taasisi ya Saratani Ocean Road Jijini Dar es Salaam. 

“Wataalamu wanatueleza kwamba mtu anaweza kujichunguza mwenyewe na akiona mabadiliko ya uvimbe katika titi, basi anashauriwa kuwahi katika kituo cha kutolea huduma za Afya kwa uchunguzi zaidi”. Amesema Waziri Ummy 

Aidha, Waziri Ummy amesema Tanzania inakadiriwa kuwa na wagonjwa wapya wa Saratani takribani Elfu Arobaini na Mbili (42,000) kila Mwaka ndio wanafika katika vituo vya kutolea huduma za Afya. 

“Wakati Tanzania tunakadiriwa kuwa na wagoniwa wapya wa Saratani takribani Elfu Arobaini na Mbili (42,000) kila Mwaka, wagonjwa asilimia 38 tu ndio wanafika Hospitali, maana yake katika kila wagonjwa 100 wa Saratani, wagonjwa 38 tu ndio wanafika katika vituo vya kutolea huduma za Afya". Amesema Waziri Ummy 

Pia, Waziri Ummy amesema taarifa ya mwaka 2022/2023, inaonesha kuwa Taasisi ya Saratani Ocean Road ilihudumia wagonjwa wapya takriban 8,779 na asilimia 13 ya wagonjwa hao sawa na wagonjwa 1,141 walikuwa na Saratani ya Matiti.

Sambamba na hayo, Waziri Ummy amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuiwezesha Wizara ya Afya kufunga mashine za CT-Scan katika Hospitali zote za Rufaa za Mikoa na mashine za Ultrasound katika Hospitali zote za Halmashauri nchini. 

“Hii inamaanisha uchunguzi na ugunduzi wa Saratani ya Matiti ambapo unaweza kupima katika Hospitali ambazo zipo karibu na mahali tunapoishi ikiwemo Hospitali za Rufaa za Mikoa na Hospitali za Halmashauri”. Amesema Waziri Ummy 

Hivyo, Waziri Ummy ametoa wito kwa wananchi kuhakikisha wanafanya vipimo katika Hospitali angalau mara moja kwa mwaka hasa kwa wanawake endapo ikigundulika una tatizo basi matibabu yaanze mapema. 

“Lakini hata wanaume wanatakiwa kupima kwakuwa, katika kila wagonjwa wa Saratani ya Matiti 100, wagonjwa 99 ni wanawake na Mmoja ni mwanaume hivyo tunawaomba wananchi wawahi katika vituo vya kutolewa huduma za Afya ili kupima na kupata matibabu mapema kwa wenye changamoto hiyo”. Amesema Waziri Ummy