Back to top

WATOTO WOTE WANAOZALIWA WAPIMWE SIKOSELI - WAZIRI UMMY

02 October 2023
Share

Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amezitaka Hospitali zote za Halmashauri nchini kuwapima ugonjwa wa Sikoseli watoto wote wanaozaliwa katika Hospitali hizo ili kujua Hali zao mapema na kuanza matibabu. 

Waziri Ummy ameyasema hayo leo Octoba 2,2023 wakati akizindua kampeni ya kuelimisha jamii juu ya Magonjwa Yasiyoambukiza yaliyofanyika katika Hospitali ya Sinza - Palestina Jijini Dar es Salaam.

“Waganga Wakuu wa Mikoa mkalisimamie hili nataka Hospitali zote za Halmashauri nchini ndani ya Miezi Sita zipime ugonjwa wa Sikoseli kwa watoto wanaozaliwa katika Hospitali hizo kabla sijashuka vituo vya Afya”. Alisema Waziri Ummy Mwalimu

Waziri Ummy amebainisha kuwa zaidi ya asilimia 70 hadi 90 ya watoto wanaozaliwa na Sikoseli hupoteza maisha ndani ya kipindi cha Miaka Mitano ya mwanzo wa maisha yao kutokana na kutotambulika au kwa sababu ya unyanyapaa na kukosa elimu.

“Hali hii haikubaliki ni lazima tuchukue hatua za haraka ili kuokoa maisha ya watoto wachanga wenye ugonjwa wa Sikoseli kwa kuwatambua mapema ili kuhakikisha wanapata matibabu kwa wakati" Alisema Waziri Ummy Mwalimu

Waziri Ummy amesema kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan anatoa fedha za dawa kwa asilimia 100 kila mwezi, fedha hizo wanaruhusiwa kuzitumia kwa ajili ya kununua mashine za kupima ugonjwa wa Sikoseli.