Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mh Mwanaidi Ali Khamis amemwagiza Mkuu wa Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu, Bw.Aswege Kaminyoge achunguze gharama zilizotumika kujenga jengo la utawala la miradi ya kimkakati ya Chaki na Vifungashio wilayani humo, baada ya kutoridhishwa na gharama zilizotumika ikilinganishwa na jengo hilo lilivyo.
.
Aametoa agizo hilo mjini Maswa, baada ya kukagua ujenzi wa miundombinu ya miradi hiyo inayofadhiliwa na Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango kwa gharama ya zaidi ya shilingi bilioni nane.
.
Amesema jengo hilo lililokamilika kwa asilimia 93 ni la kawaida sana na haliwezi kugharimu shilingi milioni mia moja sabini na nane fedha ambazo amesema ni nyingi ikilinganishwa na thamani ya jengo hilo ambalo mpaka sasa limejengwa kwa gharama ya shilingi milioni mia moja na kumi kwa kutumia mfumo wa Force Account.
.
Aidha, amemuagiza Mkandarasi wa SUMA JKT anayesimamia ujenzi wa Kiwanda cha Chaki na vifungashio ahakikishe ujenzi wa majengo ya mradi huo yanakamilika ifikapo tarehe 15 mwezi Januari, 2021 kama alivyoelekeza Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mheshimiwa Selemani Jafo, ili kazi ya kufunga mitambo ya kiwanda hicho ifanyike na kuanza uzalishaji.