
Mahakama ya Hakimu mkazi Kisutu imepanga kutoa uamuzi kuhusu kuendelea kuwepo ama kutokuwepo na dhamana kwa Mwenyekiti wa chama cha demokrasia na maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe na Mbunge wa Tarime mjini, Ester Matiko Jumatatu ijayo, Novemba 23, 2018.
Mahakama hiyo imepanga kutoa uamuzi huo tarehe hiyo baada ya kumaliza kusikiliza utetezi wa Mbowe na Matiko kwa nini wasifutiwe dhamana kutokana na kushindwa kufika mahakamani kisikiliza kesi yao ya jinai inayowakabili mahakamani hapo, Novemba 8, mwaka huu.
Mbowe, Matiko na viongozi wengine wa Chadema wanakabiliwa na kesi ya jinai pamoja na mambo mengine wakikabiliwa na mashtaka ya uchochezi na uchochezi wa uasi na kuhamasisha wafuasi wao kutembea na silaha mitaani.
Walitakiwa kufika mahakamani novemba 8 kusomewa maelezo ya awali lakini hawakufika ndipo Hakimu mkazi mkuu, Wilbard Mashauri anayesikiliza kesi hiyo alipotoa amri ya kuwakamata na kuwafikisha mahakamani wajieleze ni kwa nini wasifutiwe dhamana.
Lakini washtakiwa hao wamefika mahakamani wenyewe kabla ya kukamatwa na kutoa utetezi wao, ambao hata hivyo umepingwa vikali na upande wa mashtaka, ukiongozwa na wakili wa serikali mkuu Faraja Nchimbi, akisaidiana na Dk Zainabu Mango na wakili wa serikali Jackline Nyantori.