Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amemuagiza Mkurugenzi wa jiji la Dodoma, Godwin Kunambi kuendelea kutenga maeneo ya mapumziko ili wananchi wapate sehemu za kukutana na kubadilishana mawazo baada ya kumaliza kufanya kazi.
Ametoa kauli hiyo leo alipotembelea Mradi wa Uendelezaji wa Miji ya Kimkakati katika jiji la Dodoma na kukagua ujenzi wa maegesho ya malori makubwa katika eneo la Nala na uboreshwaji wa mandhari ya eneo la kupumzikia la Chinangalijijini Dodoma.
Waziri Mkuu amekagua maeneo hayo leo (Jumamosi, Desemba 29, 2018) ambapo ameupongeza uongozi wa jiji la Dodoma kwa kubuni wazo hilo na kusema kwamba ni muhimu kwa miji mikubwa kutenga maeneo ya kwa ajili ya mapumziko.
Amesema lazima jiji la Dodoma lipangwe kisasa na amewataka wahandisi wahakikishe maeneo ya mapumziko yatengwa na yanatumika kama ilivyokusudiwa. Pia amemtaka Mkurugenzi wa Jiji, Kunambi aendelee kusimamia ujenzi wa kimkakati ndani ya jiji hilo.