Back to top

MAKANDARASI WAFUNDWA USIMAMIZI MIKATABA MIRADI YA UJENZI

26 July 2024
Share

Makandarasi wameaswa kuzisimamia kampuni zao vizuri na kuzingatia misingi ya Usimamizi wa Mikataba katika utekelezaji wake.

Amewaaswa kutumia wataalamu wa fani stahiki katika makampuni yao na katika utekelezaji wa miradi, ili kuepuka changamoto zinazoweza kuathiri utendaji wa makampuni yao au utekelezaji wa miradi.

Akizungumza katika mafunzo hayo yaliyofanyika kwa siku tatu mkoani Dodoma, Mratibu wa mafunzo, Mkuu wa Idara ya Utafiti na Maendeleo kwa Makandarasi, Mhandisi. David Jere, alisema kuwa lengo ni kuwajengea uwezo na kukuza ujuzi kwa makandarasi pamoja na waajiri kuhusiana na namna nzuri ya kusimamia mikataba ya kazi za ujenzi.

Sambamba na hayo alisisitiza kuwa makandarasi washiriki mafunzo mbalimbali yanayoandaliwa na CRB ili kuwaongezea thamani kwasababu ujuzi huwa unaongeza ufanisi katika shughuli yoyote ile na wafanye kwa vitendo yale yote waliyofundishwa, kushirikiana   na kutimiza wajibu wao katika miradi mbali mbali na kuwa wafanyabiashara wa kweli na halali bila kukwepa kulipa kodi, kughushi nyaraka na kufanya kazi kwa weledi na kwa kuzingatia sheria za nchi.

Mhandisi Mshauri, Alex Kijugo kutokea RUWASA alisema amefurahishwa na mafunzo hayo kwani yamemuwezesha kujua majukumu yake ipasavyo kwa kutofautisha baina ya majukumu ya Mkandarasi na Mshauri.

Hata hivyo Kijugo alisema muda, ubora wa kazi na gharama zake ni mambo ya muhimu aliyoyachukua zaidi katika kuhakikisha anakwenda kusimamia ipasavyo katika suala zima la usimamizi wa Mikataba.

Kwa upande wake Gunilla Nyagawa, Meneja wa Shughuli kutokea Africentric Company Ltd aliishukuru Bodi kwa kuwezesha utolewaji wa kozi maalumu ya Mafunzo ya Usimamizi wa Mikataba kwa Makandarasi, nakusema kuwa imempa mwanga mzuri wa namna sahihi na bora wakati wa kutekeleza majukumu yake ya ukandarasi.

Aidha, Nyagawa alisema jambo lingine ambalo limekuwa ni msaada kupitia mafunzo hayo ni hali ya kupata majibu ya mambo ambayo yamekuwa na changamoto wakati wa kutekeleza majukumu yao na hivyo kupitia wataalamu husika ambao ni wawezeshaji wamekuwa ni msaada mkubwa kwao.

Mwisho Nyagawa alitoa rai kwa Makandarasi kuzichangamkia fursa mbalimbali za mafunzo yanayokuwa yakiandaliwa na Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB) ili kujengewa uwezo mzuri utakaowasaidia wakati wabutendaji kazi wao.

Mafunzo haya yamewakutanisha washiriki zaidi ya 90 kutoka mikoa 13 hapa nchini wakiwemo Makandarasi na Waajiri.