Back to top

Migogoro mikubwa 14 kati ya 29 ya wakulima na wafugaji yatatuliwa.

22 March 2019
Share

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe.Abdallah Ulega amesema wizara kupitia timu yake maalum ya kushughulikia migogoro, hadi sasa imetatua migogoro mikubwa 14 kati ya 29 inayohusisha wakulima na wafugaji pamoja na hifadhi na wawekezaji.

Naibu Waziri Ulega amebainisha hayo alipokuwa akizungumza na Mkuu wa Wilaya ya Hai Mkoani Kilimanjaro Mhe.Lengai Ole Sabaya pamoja na viongozi wengine wa wilaya hiyo, mara baada ya kuarifiwa kuwepo kwa mgogoro wa wakulima na wafugaji katika Wilaya ya Hai na kubainisha kuwa ni hatari kwa jamii inayoishi pamoja kuwa na mgogoro wa aina hiyo.

Ulega amesema atamsisitiza katibu mkuu mifugo aliangalie kwa karibu sana jambo hilo kwa sababu ni hatari sana kwa jamii inayoishi pamoja kutokuwa na maelewano ya kuachiana maeneo kwa ajili ya shughuli zao za kiuchumi.

Mhe.Ulega ametoa kauli hiyo baada ya Mkuu wa Wilaya ya Hai Mhe.Lengai Ole Sabaya kumuarifu kuwa baadhi ya maeneo yenye migogoro ni Kata ya KIA ambapo wafugaji wamekuwa wakiingiza mifugo yao katika maeneo ya uwanja wa ndege wa KIA, pamoja na wakulima wilayani humo kutotaka kuwaachia wafugaji maeneo wasiyoyatumia kwa kilimo hususan yenye magadi kwa ajili ya malisho kwa wafugaji hivyo kutengeneza chuki dhidi yao.

Mheshimiwa Ulega amemshauri pia mkuu huyo wa wilaya kutumia Chuo cha Mifugo Tengeru na Kituo cha Uhimilishaji cha Taifa (NAIC) vilivyopo Mkoani Arusha ili kuleta mabadiliko kwa wafugaji katika Wilaya ya Hai Mkoani Kilimanjaro kwa kuwa na ng'ombe wachache na wenye tija ukizingatia ukanda huo kuna kiwanda cha maziwa cha Tanga Fresh ambacho kinahitaji maziwa kwa wingi katika uzalishaji wao.