Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. David Silinde, ameongoza paredi ya 12 ya mifugo iliyofanyika kwenye viwanja vya Maonesho ya Nanenane, Kanda ya kati Jijini Dodoma, ambapo Ngo’mbe wa nyama na maziwa kutoka kwenye Taasisi mbalimbali za Serikali na sekta binafsi, wameshindanishwa kwa lengo la kuhamasisha ufugaji wa kisasa nchini.
Kwenye hotuba yake wakati wa paredi hiyo mbali na kuwapongeza wafugaji waliojitokeza kushindanisha mifugo yao, amesema kuwa paredi hiyo huwasaidia wafugaji kuongeza ari na tija ya kuongeza uzalishaji kwa kutumia teknolojia zinazokidhi mahitaji ya soko.
“Kuendelea kufanyika kwa maonesho haya ya paredi ya mifugo kumechangia mabadiliko makubwa kwenye sekta ya mifugo hapa nchini hivyo kwa sasa Wizara inaangalia uwezekano wa kufanya yawe na taswira ya kitaifa kama ilivyokusudiwa ambapo wafugaji walioshinda katika kanda mbalimbali watakuja Dodoma ili kupata mshindi mmoja wa kitaifa” Ameongeza Mhe. Silinde.
Aidha Mhe.Silinde amebainisha kuwa Wizara itaendelea kuongeza thamani ya zawadi kwa washindi ili kuendelea kuhamasisha wafugaji wengi zaidi kushiriki paredi hiyo ambapo aliwasisitiza wafugaji kuendelea kufanya ufugaji wenye tija na wa kibiashara ili kuongeza ajira, kipato, kupiga vita umasikini na kuchangia uchumi wa nchi.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule ameipongeza Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa ubunifu huo ambapo ameongeza kuwa unachangia kuongeza hamasa kwa wafugaji wa ng’ombe wa nyama na maziwa nchini kuboresha shughuli zao za ufugaji.
“Kuna paredi ya Mifugo na mnada wa nyama choma ambavyo vyote vinafanywa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwenye Maonesho ya NaneNane kanda ya kati na hivyo ni vitu vikubwa ambavyo vinawavutia watu wengi kufika kwenye haya maonesho kila mwaka” Aliongeza Mhe. Senyamule.
Awali akiwakaribisha wananchi kwenye Paredi hiyo, Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Charles Mhina amesema kuwa Maonesho hayo ni jitihada za Wizara yake kuenzi mawazo ya aliyekuwa Rais wa awamu ya 4 wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Jakaya Kikwete ambaye aliasisi paredi hiyo kwenye kilele cha Maonesho ya NaneNane mwaka 2011.
Mshindi wa Paredi hiyo anatarajiwa kutangazwa wakati wa Kilele cha Maonesho ya NaneNane mwaka huu kitakachofanyika Agosti 8, 2023.