Back to top

WADAU WA AFYA LIPENI MADENI MNAYODAIWA NA MSD

29 June 2024
Share

Wadau wa afya wanaodaiwa na Bohari ya Dawa (MSD), katika mikoa ya Kagera na Geita, wametakiwa kulipa madeni wanayodaiwa ambayo yanakadiriwa kufikia shilingi bilioni 6.5, ili kuiwezesha MSD kutekeleza majukumu yake kwa weledi, katika kununua, kutunza, na kusambaza bidhaa za afya, sambamba na kulipa washitiri wanaofanya nao biashara.

Hayo yameelezwa na Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Bw.Erasto Sima, wakati akifungua mkutano wa mwaka wa MSD na Wateja wake, wa mikoa ya Kagera na Geita, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera, uliofanyika katika Ukumbi wa ELCT uliopo Manispaa ya Bukoba ambapo ameeleza kuwa limbikizo kubwa la madeni linalodaiwa na MSD kwenye vituo vya kutolea huduma za afya, unaathiri kwa kiasi kikubwa utendaji kazi wa Taasisi hiyo, hali inayokwamisha uwezo wake kutoa huduma.

Pia, Mkuu huyo wa Wilaya ya Bukoba, amewataka wadau hao kuendelea kushirikiana na Taasisi ya MSD kwa kuboresha mahusiano na mawasiliano, ili kwa pamoja waweze kujadiliana na kutatua changamoto mbalimbali zinazo wakabili.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Ugavi na Uendeshaji wa MSD Victor Sungusia, amesema MSD imefanya maboresho huduma zake kwa kiasi kikubwa, ikiwemo upatikanaji wa bidhaa za afya ambapo hivi sasa uwezo MSD kukidhi mahitaji ya wateja wake upanda kutoka 40% kwa mwaka 2021/2022, hadi kufikia asilimia 80% kwa mwaka 2023/2024, jambo ambalo limepunguza uhaba wa bidhaa na malalamiko ya wateja.