Back to top

MTANDA APONGEZA DCEA KWA KAZI NZURI

28 June 2024
Share

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Said Mtanda, amefungua rasmi Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kupiga Vita Dawa za Kulevya yaliyofanyika jijini Mwanza. 
 
Katika hotuba yake ya ufunguzi, Mhe. Mtanda ameipongeza Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) kwa kazi nzuri wanayofanya katika kudhibiti uuzaji, usambazaji na utumiaji wa dawa za kulevya nchini. Amesema kuwa jitihada za DCEA zimechangia kupunguza kwa kiasi kikubwa matumizi ya dawa za kulevya, jambo ambalo limeleta mabadiliko chanya katika jamii. 
 
Mhe. Mtanda amewataka wananchi kuendelea kushirikiana na DCEA katika vita dhidi ya dawa za kulevya kwa kutoa taarifa za watu wanaohusika na biashara haramu ya dawa hizo. Amewataka pia wazazi kuwa waangalifu na watoto wao na kuhakikisha kuwa hawaingii kwenye matumizi ya dawa za kulevya. 
 
Maadhimisho ya mwaka huu yanafanyika chini ya kauli mbiu ya "Wekeza Katika Kinga na Tiba Dhidi ya Dawa za Kulevya." Kauli mbiu hii inasisitiza umuhimu wa kuzuia matumizi ya dawa za kulevya kwa vijana na kutoa huduma bora za matibabu kwa watu wanaotumia dawa hizo. 
 
Maadhimisho hayo yameambatana na shughuli mbalimbali zikiwemo maonyesho ya bidhaa za DCEA, mihadhara ya kuelimisha kuhusu madhara ya dawa za kulevya, na michezo.