Wakina mama wajawazito waliopo kijiji cha Pozo huko wilayani Handeni mkoani Tanga wamesema wanalazimika kupata vipimo vyao wakiwa juu ya viti vya mbao kutokana na kijiji chao kukosa zahanati jambo ambalo linasababisha baadhi yao kukosa huduma hiyo kutokana na kutolewa sehemu za uwazi hali inayosababisha baadhi yao kuona aibu kuhudhuria kliniki.
Wakina mama hao wameyasema hayo mbele ya mkuu wa wilaya Mhe.Toba Nguvile wakati alipo fanya ziara kijijini hapo yenye lengo la kusikiliza kero zinazowakabili wananchi na huku pia ikiwa ni moja kati ya ziara ya kujitambulisha kwa wananchi hao toka pale alipoteuliwa kuwa mkuu wa wilaya.
ITV imeongea na muuguzi kutoka zahanati ya Kwamsisi ambayo ipo umbali wa zaidi ya kilomita kumi na tano na amedai kuwa wanafika kijijini hapo kwa wiki mara moja ili kuwahudumia wakina mama hao lakini changamoto ni mahala pa kutolea huduma hiyo kwani wanalazimika kuomba nyumba ya mtu jambo ambalo kitaalam sio sahihi.