Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega, amesema katika mwaka huu wa fedha wa 2024/2025, wizara yake itanunua ndege nyuki ambazo zitasaidia kupambana na uvuvi haramu ikiwemo pia kufanya doria za mara kwa mara katika Ziwa Victoria.
Waziri Ulega ameleza aya alipokutana na Wadau wa Uvuvi wa Kanda ya Ziwa Victoria Jijini Mwanza Oktoba, kwa lengo la kusikiliza kero zao na kujadiliana nao masuala mbalimbali ya maendeleo yanayohusu shughuli za uvuvi katika ziwa hilo.
Pamoja na mambo mengine, wadau hao wameonesha kutofurahishwa na vitendo vya uvuvi haramu vinavyoendelea kufanywa na baadhi ya wavuvi katika ziwa hilo, huku wakimuomba Waziri Ulega na wizara yake, kuhakikisha wanachukua hatua kali za kuukomesha kwasababu unatishia mustakabali wa rasilimali za uvuvi ziwani humo.
Waziri Ulega amewahakikishia wadau hao kuwa Serikali ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, iko imara na ni sikivu, na kwamba inaendelea kutekeleza mikakati kadhaa ya kuhakikisha vitendo vya uvuvi haramu vinakomeshwa.
Kwa nyakati tofauti, wadau hao wa uvuvi hawakusita kumshukuru Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuwawezesha mikopo nafuu ya vizimba na maboti wakieleza kuwa hatua hiyo imekuwa mkombozi kwao kwani wameshaanza kuona matunda yake.
Katika kuhakikisha rasilimali za uvuvi zinakuwa endelevu kwenye ziwa hilo, Waziri huyo amewaeleza wadau hao kuwa Serikali ya Rais Samia kwa kushirikiana na Benki ya Dunia, itanunua maboya takriban 100 kwa ajili ya kuyaweka katika maeneo ya mazalia ya samaki kwa lengo la kulinda mazalia hayo dhidi ya wavuvi haramu.
Vilevile, amewataka maafisa uvuvi kutimiza wajibu wao katika kuhakikisha vitendo vya uvuvi haramu vinakoma katika maeneo yao wanayoyasimamia ili shughuli hizo ziendelee kuwa na tija kwa jamii.
Halikadhalika, aliwahakikishia wavuvi hao kuwa serikali kupitia wizara yake itaendelea kuwawekea mazingira wezeshi ikiwemo kuendelea kuwapatia mikopo nafuu ya vifaa ili wavuvi hao waweze kuboresha shughuli zao.
Mkutano huo ulihudhuliwa na wadau wa uvuvi wanaohusika na mnyororo mzima wa thamani kutoka katika mikoa iliyopo katika ukanda huo wa ziwa ikiwemo Mwanza, Geita, Kagera, Mara na Simiyu.