Back to top

Waziri Mbarawa ameiagiza MWAUWASA kutumia mfumo mpya wa mita.

16 August 2018
Share

 
Waziri wa Maji na Umwagiliaji Prof.Makame Mbarawa amewaagiza watendaji wa mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira jijini Mwanza ( MWAUWASA ) kutumia mfumo mpya wa mita za malipo ya kabla kupunguza malalamiko kwa wateja na kuongeza kasi ya usambazaji wa maji kwa wananchi wa jiji hilo ili kuongeza makusanyo ya serikali kutoka shilingi Bilioni 2.3, ambazo mamlaka hiyo inazikusanya kwa mwezi hadi kufikia shilingi Bilioni 2.8 kuanzia mwezi ujao wa septemba mwaka huu.
 
Waziri mbarawa ametoa agizo hilo baada ya kuzindua jingo jipya la kisasa la mamlaka hiyo lenye ghorofa tano ambalo limejengwa kwa gharama ya zaidi ya shilingi Bilioni 7 zikiwa ni fedha za ndani na mkandarasi kampuni ya D.F Mistry ya jijini Mwanza, ambapo amewaagiza watumishi wa MWAUWASA kuanza kuwafuata majumbani wateja wao ili kuwaunganishia maji katika jitihada za kuongeza maduhuli ya mamlaka hiyo.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya majisafi na usafi wa mazingira jijini Mwanza Mhandisi Anthony Sanga, amemhakikishia Waziri prof. Mbarawa kwamba licha ya mamlaka hiyo kuwa na mipango madhubuti ya kufikisha huduma ya maji hasa kwa wananchi wanaoishi maeneo ya milimani na miinuko jijini humo, pia MWAUWASA imejipanga kuhakikisha inatatua baadhi ya changamoto zinazowakabili wateja wao.