Uzalishaji wa mazao ya nafaka katika wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma umeongezeka kutoka wastani wa gunia mbili hadi wastani wa gunia 18 za mahindi kwa ekari moja, baada ya wakulima kuanza kulima kisasa na kutumia mbinu bora za kilimo licha ya wakulima kulalamikia upatikanaji na bei kubwa ya pembejeo hasa mbolea.
Wakizungumza na ITV katika vijiji vya Nyumbigwa, Kanazi, Murufiti, Kigondo, Nyansha na Nyakitonto wakulima wameeleza kuwa mabadiliko hayo yametokana na kuanzishwa kwa vikundi vya wakulima vijijini kupitia mradi wa tija Tanzania unaofadhiliwa na taasisi inayochochea kilimo chenye tija (AGRA) ambapo wameweza kuhamasishwa na kuanza kutumia pembejeo kwa kuzingatia utaalam.
Kwa upande wake afisa mradi wa pata tija Tanzania katika mkoa wa Kigoma Donald Mizambwa amesema lengo la mradi huo ulioanza mwaka juzi ni kuongeza tija kutokana na wakulima kulima kisasa katika eneo dogo huku kaimu afisa kilimo katika halmashauri ya wilaya ya Kasulu Faidaya Misango akieleza kuwa pamoja na maafisa ugani wa mradi huo kusaidia wakulima,wakulima wameanza kubadilika kutoka kulima kienyeji na kuanza kulima kisasa hali ambayo inaleta tija.