Wachimbaji wadogo wa madini aina ya chokaa katika tarafa ya Makere wilayani Kasulu mkoani Kigoma wamelalamika kuondolewa katika maeneo ya hifadhi na kusababisha zaidi ya wachimbaji mia nne kuacha kazi hiyo.
Wachimbaji hao wamemweleza waziri wa madini Mhe.Dotto Biteko kuwa katika tarafa hiyo madini aina ya chokaa yanapatikana ndani ya hifadhi ya msitu wa Makere kusini na kwamba awali walikuwa wanachimba kulingana na taratibu zilizowekwa lakini kwa sasa wameondolewa hali ambayo imesababisha hasara na watu wengi kukosa kazi ilhali shughuli yao haiharibu mazingira.
Kwa upande wake waziri wa madini Mhe.Dotto Biteko ameitaka wakala wa misitu Tanzania TFS kukutana na maafisa wa wizara ya madini ili kuona namna ya kuwasaidia wachimbaji ambao wamefuata taratibu ili kuchimba madini ndani ya msitu huo kwa kuwa inawezekana suala hilo kufanywa kwa mujibu wa utaratibu.