Siku chache baada ya watu wanaodaiwa kuwa wafuasi wa Meya wa Halmashauri ya jiji la Mwanza James Bwire, kufanya fujo na kuvunja mkutano wa Naibu waziri wa nchi ofisi ya rais TAMISEMI Mhe. Mwita Waitara uliofanyika katika zahanati ya Mahina jijini humo, jeshi la polisi mkoani Mwanza limemkamata meya huyo kwa ajili ya mahojiano.
Kamanda wa polisi wa mkoa wa Mwanza Muliro Jumanne Muliro amethibitisha kushikiliwa kwa meya huyo ambaye ni diwani wa kata ya Mahina, anayetuhumiwa kuandaa kikundi cha watu kufanya fujo kwenye mkutano wa naibu waziri huyo mei 27 mwaka huu.
Mh .Mwita Waitara, mei 27 mwaka huu akiwa katika zahanati ya kata ya Mahina kukagua mradi wa ujenzi wa wodi ya wazazi, alishindwa kuendelea na mkutano wake baada ya kikundi cha watu wachache kuanzisha vurugu wakati akisoma barua ya mkuu wa wilaya ya Nyamagana kuhusiana na mgogoro wa eneo la umma lililopo katika eneo la zahanati hiyo ambalo linadaiwa kuchukuliwa na uongozi wa shule za Alliance.
Hii ni mara ya pili kwa meya wa Mwanza James Bwire kukamatwa na polisi tangu aingie madarakani novemba 2015, mara ya kwanza ilikuwa ni Oktoba 30 mwaka 2017 wakati wa ziara ya rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli ambapo alikamatwa akiwa katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mwanza kwenye mapokezi ya rais.