
Bodi ya Korosho Tanzania imetoa leseni maalum kwa wataalam wanaosimamia ubora wa zao hilo katika maghala makuu, ili kukabiliana na tatizo la korosho zisizokidhi ubora lililojitokeza msimu uliyopita na kuleta hasara kwa wakulima.
Kaimu Mkurugenzi wa Masoko wa bodi hiyo Domina Mkangalla amesema hayo wakati wa kutoa elimu ya zao la korosho ili kuhakikisha korosho zitakazopelekwa sokoni katika msimu wa mwaka huu ziwe na ubora unaokubalika katika masoko.
Amesema katika msimu wa mwaka jana ni asilimia themanini na nane pekee zilipatikana na korosho za daraja la kwanza na korosho zilizobaki zikiwa na ubora wa daraja la pili na zingine zikiwa na ubora wa chini ambao ni vigumu mkulima kupata bei nzuri sokoni.
Amesema kati ya mikoa iliyopata korosho zenye ubora usiofaa ni pamoja na mikoa ya Tanga na Pwani, hivyo bodi hiyo isingependa kuona hali hiyo ikijirudia.
Amesema leseni hiyo itawezesha kuweka usimamizi mzuri wa zao hilo katika maghala hayo ambayo yamekuwa yakilalamikiwa na wanunuzi wa korosho kwa kuhifadhi korosho zisizo na ubora.