Watendaji wakuu na wafanyabiashara wenye pato linaloanzia Shilingi Bilioni moja nchini wamepewa 'Tuzo za Wakuu na Watendaji Wa Kampuni 100 Bora Tanzania' ambazo zinatajwa kuwa chachu ya Maendeleo nchini kwa kuendelea kufanya kazi zaidi katika kuchochea ufanisi wa kazi.
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Eastern Star, Deogratius Kilawe, wakati wa utoaji wa tuzo hizo uliofanyika Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na watendaji na wakuu wa kampuni mbalimbali nchini.
Mbali ya tuzo hizo kutolewa kwa kigezo cha mapato ya biashara, pia huzingatia mchango wa biashara hizo kwenye ukuaji wa uchumi wa taasisi hizo, wananchi na nchi kwa ujumla.
"Tumefanya utafiti yakinifu na wa kina, ili kuwapata wakuu na watendaji wa kampuni 100 bora nchini, Tunaamini kupitia mchakato huu tutasaidia kutoa fursa kwa washiriki hao kunufaika zaidi' Ameongeza Kilawe
Tuzo hizo za wakuu na watendaji wa kampuni 100 bora 'Tanzania Top 100 Executive Awards' zimefanyika kwa msimu wa tatu kwa lengo la kuwatambua watendaji wakuu wa kampuni mbalimbali wanaofanya vizuri nchini ili kuendelea kuongeza chachu ya ufanisi kwenye biashara.