Back to top

GRIDI YA TAIFA KUMALIZA TATIZO LA UMEME RUKWA

25 June 2024
Share

Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga amesema changamoto ya umeme katika  Mkoa wa Rukwa itamalizika baada ya Mkoa huo kuunganishwa  katika Gridi ya Taifa kupitia Mradi wa njia ya kusafirisha Umeme wa Msongo wa Mkubwa wa Kilovolti 400 wa Tanzania - Zambia (TAZA). 

Mhe. Kapinga amesema hayo leo Juni 26, 2024 Bungeni Jijini Dodoma alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Nkansi, Mhe. Aida Khenani aliyetaka  kufahamu mpango wa Serikali wa kumaliza changamoto ya umeme Wilaya ya Nkansi.

 Amesema kupitia mradi huo kitajengwa Kituo vya Kupokea na Kupoza umeme cha Nkansi ambacho kitasaidia kuboresha upatikanaji wa umeme katika Wilaya hiyo na maeneo jirani.
 
Kuhusu mabadiliko ya bei za umeme katika Mamlaka za Miji Midogo za Namanyere na Laela, amesema kuwa Serikali imefanya mapitio na imeshauri kuwa maeneo 1,500 yamekidhi kulipia kiasi cha shilingi   27,000 badala  320,000.

Vilevile  Serikali inaendelea  kufanya mapitio katika maeneo mengine ya Miji hiyo ili kujiridhisha kama yanakidhi vigezo husika na  ili yaingizwe  kwenye malipo ya shilingi 27,000/-.

Kuhusu utekelezaji wa mradi  wa TAZA, amesema kuwa,  Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati,  Mhe. Dkt.  Doto Biteko alifanya ziara katika mradi huo na kwamba utekelezaji wake unaenda kwa kasi na Serikali inaendelea kumsimamia Mkandarasi anayetekeleza mradi huo ili ukamilike kwa wakati. 

Amesisitiza kuwa adhma ya Serikali ni kuyafikishia umeme maeneo yote muhimu zikiwemo Taasisi zilizopo umbali usiozidi mita 500 kutoka ilipo miundombinu ya umeme na kuongeza kuwa maeneo ambao yapo mbali na miundombinu hiyo yatafikiwa kupitia miradi ya vitongoji.