
Chama cha Mapinduzi Manispaa ya Moshi kimelilalamikia Jeshi la Zima Moto na Uokoaji Mkoani Kilimanjaro kwa kushindwa kuwahudumia wananchi katika majanga ya moto yanapotokea na kuwasababishia hasara kubwa ya nyumba na mali zao kwa kutofika kwa wakati maeneo ya matukio.
Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi wa manispaa hiyo,Alhaji OMARI AMINI SHAMBA ametoa lawama hizo kufuatia kuungua moto nyumba ya Bi ANNA MZIRAY,katika Kata ya Njoro ambayo jeshi hilo lilishindwa kufika kwa wakati ingawa walipewa taarifa baada ya moto huo kuzuka saa nane na nusu usiku.
Alhaji SHAMBA ameiomba serikali kuchukua hatua za haraka dhidi ya jeshi hilo ambalo linaifedhehesha serikali huku nyumba za wananchi na mali zao zikiendelea kuteketea mara kwa mara ili isiendelee kutokea.
Mwenyekiti wa mtaa wa viwanda katika kata hiyo,Bwana OSWALD KIMBI amesema,hii ni mara ya tatu kwa nyumba kuungua katika mtaa huo,lakini jeshi la Zima Moto limekuwa likishindwa kufika kuokoa nyumba na mali za wananchi.
Kamanda wa jeshi hilo Mkoani Kilimanjaro,Bwana BARAKA MVANO amesema kwa sasa gari lao ni bovu na lipo kwenye matengenezo na juhudi zinaendelea kulifanyia ukarabati na kupata gari lingine.