![](https://www.itv.co.tz/sites/default/files/styles/large/public/field/image/Bango.jpg?itok=4UNRQ-An)
Kaimu mkuu wa wilaya ya Dodomamjini Deogratius Ndejembi ambaye pia ni mkuu wa wilaya ya Kongwa amepokelewa na Mabango yenye jumbe mbalimbali za malalamiko yanayohusu mgogoro wa ardhi ikiwemo wananchi kupatiwa viwanja vyao wanavyodai wamedhulumiwa na uongozi wa kata ya Kikuyu kusini hali iliyozua tafrani katika mkutano wa hadhara.
Ni sehemu ya wananchi wakimpokea mkuu wa wilaya huku wakinyanyua mabango yenye jumbe mbalimbali kuhusu migogoro ya ardhi hali iliyosababisha baadhi yao kukamatwa baada ya kuanzisha fujo ambapo wananchi hao wameiomba serikali kuingilia kati mgogoro wa mashamba ambayo unaonekana kuwa kero kubwa.
Katika kutatua mgogoo huo Ndejembi ametangaza kusitisha ujenzi na kutokufanywa shughuli yoyote ya kibinadamu hadi hapo atakapokuwa amejiridhisha kwa kupata takwimu sahihi za watu wenye maeneo,na ni kwanini wamecheleweshwa kupimiwa na kupewa haki zao.
Aidha katika hatua nyingine Bwana Ndejembi ameutaka uongozi wa jiji la Dodoma kuhakikisha wanatatua migogoro hiyo ikiwa ni pamoja na kupima maeneo haraka na kutoa majibu kwa wakati kwa wananchi wa maeneo husika badala ya kuwa na mgogoro mkubwa.