Back to top

LINDENI VIUMBE BAHARINI NA KUHIFADHI MAZINGIRA

04 July 2024
Share

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt.Doto Biteko, amewataka Watanzania kulinda viumbe vya baharini na kuhifadhi mazingira ya bahari kwa ajili ya vizazi vilivyopo na vizazi vijavyo.

Dkt.Biteko amesema hayo wakati akifungua kongamano la Tatu la Uchumi wa Buluu mwaka 2024 lenye kaulimbiu, 'Kuunganisha Usalama Baharini, Utunzaji wa Mazingira na Maendeleo ya Teknolojia kwa ajili ya Ukuzaji wa Uchumi wa Buluu.

"Tunapofanya majadiliano leo, tujikite kwenye kanuni uendelevu, usawa na uvumbuzi ili hatimaye kongamano hili liwe mwanga unaotuongoza kwenye uchumi wa buluu unaoinua jamii zetu, ninawasihi kila mmoja wenu ashiriki kikamilifu ili tuweze kupata matokeo chanya ya kongamano hili" amesema Dkt. Biteko.

Amesema uchumi wa buluu unatambuliwa kama mchangiaji mkubwa wa maendeleo endelevu ambapo jamii hutumia rasilimali za bahari kwa njia ambayo ni endelevu na kwa kiasi kikubwa huzingatia uhifadhi wa mazingira.

Pia, uchumi wa buluu huchochea uvumbuzi wa fursa kama vile teknolojia ya kibayoteknolojia na nishati ya bahari, kutoa suluhu za nishati mbadala na tiba, inasaidia juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi kupitia ulinzi wa mifumo ikolojia, na kuhakikisha Ulinzi na usalama wa bahari, ambao ni muhimu kwa usalama wa usafiri wa majini na kuzuia shughuli haramu baharini.

“Pamoja na mazuri yote hayo, uchumi wa buluu unakabiliwa na changamoto kadhaa ikiwa ni pamoja na uvuvi wa kupita kiasi, uchafuzi wa bahari, mabadiliko ya hali ya hewa, uvuvi haramu, uharibifu wa makazi na kutopatikana kwa taarifa sahihi. Kama ilivyo katika nchi nyingine duniani, Tanzania pia inakabiliwa na changamoto hizo,” amesisitiza Dkt. Biteko.

Dkt. Biteko ameongeza kuwa, mwaka 1991 Tanzania ilianzisha Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI) ambapo majukumu yake ni pamoja na kushirikiana na vyuo vingine katika kufanya tafiti, kubadilishana wataalam na kutoa ushauri wa kitaalamu kwa Serikali, watu binafsi na wadau wengine kuhusiana na maswala ya bahari.