
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof.Riziki Shemdoe, amesema Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi inaendela kufanya jitihada za makusudi katika kuboresha miundombinu katika kampasi zote nane za chuo cha Wakala ya Mafunzo ya Mifugo (LITA) ambazo kwa sasa kila kampasi inaendelea na ujenzi wa miundombinu mbalimbali pamoja na ukarabati wa majengo chakavu.
Prof.Riziki Shemdoe ameeleza hayo mkoani Morogoro baada ya kuzindua bweni la wanafunzi wa kike katika chuo cha Wakala ya Mafunzo ya Mifugo (LITA) kampasi ya Morogoro lenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 216 lililogharimu zaidi ya shilingi milioni 970 fedha za mapato ya ndani
Prof. Shemdoe ameipongeza LITA kwa kufanikisha ujenzi huo kwa kutumia fedha za ndani ambapo kukamilika kwakwe kutasaidia kwa kiasi kikubwa kuondokana na changamoto ya mabweni kwa wanafunzi katika kampasi hiyo
Awali akitoa taarifa ya ujenzi wa bweni hilo Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Mafunzo ya Mifugo (LITA) Dkt.Pius Mwambene, amesema kuwa ujenzi huo umetumia miaka miwili hadi kukamilika ambapo kwa sasa wameanza kwa kujenga bweni la wanawake na kisha baadaye watahamia kwenye ujenzi bweni la wanaume
Amesema hatua hiyo ni miongoni mwa jitihada zinazofanywa na Wakala katika kutatua changamoto ya miundombinu ya kufundishia ambayo itawawezesha wanafunzi na watumishi kutekeleza majukumu yao wakiwa katika mazingira bora
Naye Mkurugenzi wa Utafiti, Mafunzo na Ugani kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Angello Mwilawa amesema Wakala unaendelea kujiandaa na utekelezaji wa mtaala mpya wa kufundishia ambao unatarajiwa kuanza kutumika mwaka mpya wa masomo mwezi octoba mwaka huu ambapo mpaka sasa wadau wawili wameshajitokeza kusadia
Amesema mtaala wa sasa unatarajiwa kufikia tamati mwezi april mwaka huu na kutoa nafasi ya kuhuisha mitaala mipya ambapo wadau waliojitokeza katika kusaidia uhuishaji wa mitaala hiyo ni pamoja na shirika la kilimo endelevu (Sustainable Agriculture Tanzania) SAT.