
Nyumba 17 zimebomoka na nyingine 20 kuezuliwa mapaa, kutokana na mvua kubwa iliyoambatana na upepo mkali katika Kijiji cha Kamsanga B, Kata ya Mnyagala, Wilaya ya Tanganyika Mkoani Katavi.
Watu watatu wamejeruhiwa katika tukio hilo akiwemo mtoto mmoja na familia kadhaa kukosa mahali pa kuishi.
Wakizungumza ITV katika kijiji hicho, wakazi hao wamesema mvua hiyo ilianza jana majira ya saa 11 jioni.
Mtendaji wa Kijiji cha Kamsanga, Bwana Mwikombe Matiku amesema licha ya wakazi wa kijiji hicho kukumbwa na taharuki, lakini walijitahidi kusaidiana.
Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika, Bwana Salehe Mhando amefika kijijini hapo na kutoa pole kwa waathirika na amewasisitiza umuhimu wa kujenga nyumba imara.