
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amehudhuria sherehe za kuapishwa kwa Mhe. Yoweri Kaguta Museveni kuwa Rais wa Jamhuri ya Uganda, zilizofanyika katika viwanja vya Kololo Jijini Kampala.
Mhe. Rais Samia amehudhuria sherehe hizo pamoja na Marais wengine 10, wawakilishi wa marais na mashirika mbalimbali ya kimataifa.
Akizungumza katika sherehe hizo, Mhe. Rais Museveni ametoa wito kwa mataifa ya Afrika kuongeza ushirikiano kwa kukamilisha itifaki ya soko la huru la Afrika ili kujihakikishia soko la ndani la bidhaa zinazozalishwa kwa wingi hasa mazao ya kilimo.
Wakati huo huo, Mhe. Rais Samia amekutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Shirikisho la Ethiopia, Mhe. Sahle-Work Zewde ambapo viongozi hao wamezungumzia kuongeza zaidi ushirikiano kati ya Tanzania na Ethiopia.
Mhe. Rais Zewde amempongeza Mhe. Rais Samia kwa kupokea kijiti cha Urais na amesema ana imani kubwa katika kipindi chake Tanzania itapiga hatua kubwa za maendeleo.
Mhe. Rais Samia pia amekutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Sudan Kusini Mhe. Salva Kiir Mayardit ambaye amempongeza kwa kupokea kijiti cha Urais na amewasilisha ombi la Sudan Kusini kupatiwa chakula kutoka Tanzania.
Kabla ya kuondoka Jijini Kampala Mhe. Rais Samia amekutana na Rais wa Jamhuri ya Uganda Mhe. Yoweri Kaguta Museveni na kumkaribisha kuhudhuria sherehe za utiaji saini mkataba kati ya Serikali ya Tanzania na kampuni za uwekezaji katika mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta ghafi la Afrika Mashariki litakalojengwa kutoka Hoima nchini Uganda hadi bandari ya Tanga nchini Tanzania, zitakazofanyika tarehe 20 Mei, 2021 Jijini Dar es Salaam.
Mhe. Rais Museveni amekubali mwaliko huo.