Back to top

WAZIRI NDEJEMBI ATAKA UADILIFU, HAKI KWA WATUMISHI SEKTA YA ARDHI

26 July 2024
Share

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe.Deogratius Ndejembi, amewataka watumishi wa sekta ya ardhi nchini, kuongeza uadilifu na kutenda haki katika utekelezaji wa majukumu yao na kuongeza kasi katika utendaji kazi.

Mhe.Ndejembi amesema suala la ardhi ni gumu na linahitaji watumishi kuwa makini, hivyo lazima watumishi wa sekta ya ardhi, watende haki huku wakizingatia kuwa kuna sheria, kanuni na miongozo inayowaoongoza katika utendaji kazi.

Mhe.Ndejembi ametoa kauli hiyo leo wakati akizungumza na viongozi pamoja na watumishi wa Wizara ya Ardhi mkoa wa Dar es Salaam mara baada ya kutoka kuapishwa, na kusema yale yote mazuri yaliyofanywa na mtangulizi wake ikiwemo Kliniki za Ardhi, atayaendendeleza kwa lengo la kuleta ufanisi wa wizara.

"Sikuja kutengua torati, yote aliyoyaanzisha mtanguluzi wangu ikiwemo klinik za ardhi zitaendelea na vile vile anayehisi jambo lake limekwama ajitokeze na atahudumiwa" amesema Mhe.Ndejembi.

Sambamba na hayo Waziri huyo wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi ametaka kuimarishwa kwa mifumo ndani ya wizara ili migogoro ya ardhi isiendelee kujitokeza.

Mhe. Ndejembi ameapishwa na Rais Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan kuwa Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi akitokea Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Watu wenye ulemavu).